Email:info@zyc.go.tz
   

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Baraza la Vijana Zanzibar

Mawasiliano - Baraza la Vijana Zanzibar

Mradi wa mabadiliko ya Tabia nchi

News Image

Mwandishi: Bahati Habibu Peter

Tarehe: Monday, 21st July 2025

BARAZA la Vijana Zanzibar limesema lina jukumu muhimu katika kuelimisha na kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za utunzaji wa mazingira.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar, Ali Haji Hassan, alisema hayo alipokuwa katika uzinduzi wa mafunzo ya mabadiliko ya tabianchi kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira, hafla ambayo ilifanyika katika Ukumbi wa Skuli ya Sekondari Tumekuja na kuhudhuriwa na Vijana na Wadau wa Mazingira.

Alisema mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inaathiri sana Vijana, Wanawake na Watoto.

Katibu huyo alifahamisha kuwa kupitia Programu hiyo, baraza linatarajia kupanda Mikoko zaidi ya 3,000 ikiwa ni hatua ya kurejesha uoto wa asili na kusaidia juhudi za kuifanya Zanzibar kuwa kijani.

Alisisitiza kuwa mradi huo unaunga mkono malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mapema akiwasilisha maelezo ya mradi huo Ofisa Mratibu wa Baraza la Vijana Zanzibar, Hemed Ramadhan Salum, alisema mradi huo unafadhiliwa na Baraza la Jiji la Zanzibar kupitia Programu ya Youth Climate Action Fund na kusimamiwa na Baraza la Vijana Zanzibar na kutekelezwa na kikundi cha “Tushikamane kwa Usafi” kutoka Shehia ya Meya.

Alisema utekelezaji wa mradi huo umeanzia toka mwezi Juni na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu na utajumuisha shughuli mbalimbali ikiwemo kupanda mikoko katika eneo la Chuini, kutoa mafunzo ya tabianchi na kuhamasisha uhifadhi na urejeshaji wa Mikoko Nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo mlezi wa Jumuiya ya Ustawi wa Jamii Shehia ya Chuini, Hussein Ali Kombo, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyatumia ipasavyo ili kuleta matokeo chanya kwa Jamii.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo walishukuru kupatiwa elimu hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wa uhifadhi wa mazingira katika maeneo yao.

Mradi huu wa “Mabadikko ya Tabianchi” unatarajiwa kutoa mwanga wa matumaini kwa Vijana wa Zanzibar, si tu kwa maendeleo ya mazingira, bali pia kwa ustawi wa jamii kwa ujumla

Taarifa za Miradi