Email:info@zyc.go.tz
   

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar

Baraza la Vijana Zanzibar

Mawasiliano - Baraza la Vijana Zanzibar

Upandaji wa Mikoko

News Image

Mwandishi: Bahati Habibu Peter

Tarehe: Monday, 21st July 2025

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vijana Zanzibar Ali Haji Hassan amewataka Vijana kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Kuifanya Zanzibar kuwa ya Kijani kwa kupanda miti ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Kauli hiyo ameitoa huko Shehia ya Chuini Wilaya ya Magharibi A katika Uzinduzi wa Mradi wa Urejeshaji wa Mikoko (Mangrove Restoration) unaofadhiliwa na Baraza la Jiji la Zanzibar kupitia Programu ya Youth Climate Action Fund na kusimamiwa na Baraza la Vijana Zanzibar na kutekelezwa na Kikundi cha Mazingira cha Tushikamane kwa Usafi Shehia ya Meya kwa Mashirikiano na Wananchi wa Shehia ya Chuini.

Amesema Vijana ni sehemu ya wanajamii hivyo wanatakiwa kufahamu na kuelewa wajibu wao katika suala zima la uhifadhi na upandaji wa mikoko katika maeneo yalioathirwa na mabadiliko ya Tabianchi .

Akizungumza na Wananchi, Wanafunzi na Vijana amewasisitiza kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika mazingira ya kila siku yanayowazunguka ili kulinda na kuhifadhi Mazingira kwa maslahi ya sasa na baadae.

"Niwaambie ikiwa kila mmoja wetu aliepo hapa atapanda mkoko mkoko mmoja na akaushughulikia ukakua huo ni sadaka yake hapa duniani na kwa mujibu wa vitabu vya dini utamfaa mti huo hata baada ya kufa" Alisema ndugu Hassan.

Akizungumza Mwenyekiti wa Mradi wa Kikundi cha Mazingira cha Tushikamane na usafi cha Shehia ya Meya Mariam Omar Hamad akielezea shughuli zitakazofanywa wakati wa kutekeleza mradi huo ni pamoja na kutoa Elimu kwa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya Tabianchi, Urejeshaji na Uhifadhi wa Mikoko pamoja na zoezi la Upandaji Mikoko katika eneo hilo la Chuini.

Aidha kutoa Elimu ya Mazingira kupitia Vipindi vya Redio, Televisheni na Mitandao ya Kijamii sambamba na kufanya tathmini na ufuatiliaji wa ukuwaji wa mikoko.

Akitoa neno la Shukran Mjumbe Shehia ya Chuini Rafii Idarous Makame amewashukuru Viongozi wa Baraza la Vijana Zanzibar kwa kuliteuwa eneo hilo kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa Urejeshaji na Upandaji wa Mikoko na kusema kuwa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo yalioathirwa na mabadiliko ya Tabianchi.

Aidha amesema kupitia Wananchi wa Shehia hiyo watahakikisha wanashirikiana kwa pamoja katika kuitunza na kuilinda Mikoko inayopandwa katika eneo inakuwa na kustawi kwa maslahi ya Vizazi vya sasa na Vizazi vya baadae.

Taarifa za Miradi